Bunge limetangaza kuwa, uchaguzi mdogo wa kupata wawakilishi wawili wa nafasi ya ubunge kwa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), sasa utafanyika Mei 10, mwaka huu kwenye ukumbi wa Bunge, mjini Dodoma.
Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu wa Bunge ambaye pia ni Msimamizi wa Uchaguzi huo, Dk Thomas Kashilillah, uteuzi wa wagombea utafanyika Mei 3.
Watakaopigiwa kura na kuchaguliwa katika uchaguzi huo wataungana na wengine saba, sita wakiwa kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mmoja kutoka Chama cha Wananchi (CUF) ambao walishinda katika uchaguzi wa Aprili 4, mwaka huu.
Siku hiyo, Chadema licha ya kuweka wagombea wao Lawrence Masha na Ezekiah Wenje, kura zao hazikutosha hivyo kukosa sifa za kuchaguliwa.
Walioshinda kwa upande wa CCM ni Fancy Nkuhi, Happiness Legiko, Maryam Ussi Yahya, Dk Abdullah Makame, Dk Ngwaru Maghembe, Alhaji Adam Kimbisa wakati kutoka CUF ni Habib Mnyaa.
0 comments:
Comment hapa