Monday, May 22, 2017

Trump: Iran haitaruhusiwa kumiliki silaha za nuklia


Iran ikionyesha silaha zake

Rais wa Marekani Donald Trump ameanza ziara yake nchini Israel kwa kuonya kuwa kuna tisho kutoka nchini Iran ikiwa itamiliki silaha za nuklia.

"Iran haitaruhusiwa kamwe kumiliki silaha za nuklia," Trump aliwaambia waandishi wa habari.
Alisafiri kutoka nchini Saudi Arabia, mshirika mkubwa wa Marekani ambapo alitoa hotuba kwa viongozi wa kiislamu.

Bw Trump anatarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa Israel na Palestina katika kipindi cha siku mbili atakazokuwa eneo hilo.

Rais huyo amesema kupatikana kwa mkataba wa amani kati ya Waisraeli na Wapalestina yatakuwa mafanikio makubwa, lakini hakusema mkataba kama huo unafaa kuchukua mwelekeo gani.

Amesema angependa sana pande zote mbili ziamue kuhusu mkataba huo wa amana kwa mashauriano ya moja kwa moja.

Katika mkutano mkuu wa viongozi wa Kiislamu na Kiarabu mjini Rihadh siku ya Jumapili, Bw Trump aliwataka viongozi hao kuwa kwenye mstari wa mbele katika kukabiliana na wanamgambo wa Kiislamu na wapiganaji wenye itikadi kali na "kuwafurusha kutoka kwenye dunia hii."

Aliitaja moja kwa moja Iran na kusema kwamba imekuwa "ikichochea mizozo ya kidini na ugaidi" katika kanda hiyo kwa miongo mingi.

Bw Trump pia alikariri tena kwamba anaamini amani kati ya Waisraeli na Wapalestina inaweza kupatikana.

Rais huyo wa Marekani amekuwa akichukuliwa sana kuwa muungaji mkono mkubwa wa Israel kuliko mtangulizi wake Barack Obama.
Source BBC


SHARE THIS

0 comments:

Comment hapa