Thursday, April 27, 2017

Raila Odinga ateuliwa na upinzani Kenya kuwa mgombea wa urais

Bw Musyoka


Muungano wa vyama vya upinzani nchini Kenya National Super Alliance (NASA) umemteua aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga kuwa mgombea wake katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Agosti mwaka 2017.

Bw Odinga sasa atakabiliana na Rais Uhuru Kenyatta atakayetumia chama cha Jubilee kuwania muhula wa pili.

"Hii ni heshima kubwa sana ambayo ndugu zangu wamenifanyia, kwa kuniweka nipeperushe bendera ya NASA.
Tumekuwa na vikao ambavyo vimechukua siku nyingi. Kila kitu tumeandika, tumekubaliana ya kwanza serikali tutakayoiunda, ambayo ni serikali ya mseto itakuwa ni serikali ya mpito," alisema Bw Odinga akihutubu baada ya kutangazwa kuwa mgombea.

Amesema atakuwa kama Joshua kwenye Biblia na kuvusha Wakenya hadi nchi ya ahadi.
"Sisi tuko kama timu, yenye pembe tano (Pentagon), wamenipa utepe wa nahodha, hiyo inaniunganisha mimi nao na Wakenya wote, tutatembea pamoja bega kwa bega. Tunataka kubadilisha Kenya na kutekeleza ndoto ya waanzilishi wa taifa letu".

Alisema serikali yake itaangazia kumaliza umasikini, kuimarisha afya, kuboresha uchumi, kubuni nafasi za kazi na kurejesha gharama ya elimu na maisha chini.

Bw Odinga pia ameahidi kuhakikisha walimu na madaktari,pamoja na wafanyakazi wengine wanalipwa mishahara mizuri.

Kadhalika, ameahidi akishinda serikali yake itamaliza rushwa serikalini.

Makamu wa rais wa zamani Musalia Mudavadi amesema viongozi wote wakuu wa muungano huo wamekubalina kumuunga mkono mgombea huyo mmoja.

"Tumekubali kwamba mpangilio huu wa uongozi ni mpangilio ambao tunataka ulinganishwe na Rasimu ya Bomas ambayo Wakenya walitaka, lakini haikuidhinishwa," amesema.

Amesema mpango wao ni kuwa wadhifa wa kinara wa mawaziri na msaidizi wake, kama ilivyokuwa kwenye rasimu hiyo ya katiba.

Mgombea mwenza wa Bw Odinga atakuwa makamu wa rais wa zamani Bw Kalonzo Musyoka, kiongozi wa Chama cha Wiper Democratic Movement.
Waziri mkuu mratibu wa shughuli za serikali atakuwa kiongozi wa chama cha Amani National Congress Musalia Mudavadi.

Naibu waziri mkuu mratibu wa uchumi atakuwa kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetangula.
Kiongozi wa Chama cha Mashinani (CCM) Isaac Ruto atakuwa naibu waziri mkuu atakayesimamia utawala na huduma za jamii."Hatutasherehekea, na bado hatujasherehekea, hadi tuing'oe serikali ya Jubilee kutoka madarakani. Ni mapema mno," alisema Bw Musyoka alipokuwa anahutubu baada ya kutangazwa kwa mgombea huyo wa urais.

"Tumegundua kwamba muhimu zaidi katika demokrasia ni kuitekeleza. Nilisema awali kwamba niko tayari kuwa hata mtu wa kufagia katika serikali ya NASA, mradu tu raia wa Kenya apate heshima yake. Wananchi wameamua huu ni mwaka wa mabadiliko. Mabadiliko hayo yanaanza nanyi (raia)."
Bw Musyoka amesema muungano wa NASA utaangazia zaidi kumaliza umaskini.

Alieleza matumaini yake kwamba mkataba wa sasa hautavunjwa, kama ilivyokuwa awali kwa makubaliano ya kugawana mamlaka katika miungano ya awali.

Amesema muungano wa sasa umefanywa wazi na kusajili kwa Msajli wa Vyama.

Mpangilio wa Upinzani
Raila Odinga - Mgombea urais
Kalonzo Musyoka - Mgombea mwenza
Musalia Mudavadi - Waziri Mkuu
Moses Wetangula - Naibu Waziri Mkuu
Isaac Ruto - Naibu Waziri Mkuu

Bw Odinga ni mwanasiasa anayesifika sana kwa ushawishi wake kisiasa na amekuwa katika msitari wa mbele kuunda vyama vya miungano na wanasiasa ambao ni mahasimu wake.

SHARE THIS

0 comments:

Comment hapa