Saturday, March 25, 2017

Stars kuikaribisha Botswana leo

TIMU ya Taifa 'Taifa Stars' leo inawakaribisha Botswana kwenye mchezo wa kimataifa wa kirafiki huku kikosi hicho cha kocha Salum Mayanga kikipanga kuwatumia wapinzani wao kama ngazi ya kupanda kwenye viwango vya ubora vya Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA).

Stars itaingia kwenye Uwanja wa Taifa ikiwa na silaha zake hatari, nahodha Mbwana Samatta na Farid Mussa wanaocheza soka Ulaya.

Akizungumzia mchezo wa leo, Kocha Mayanga, alisema wachezaji wake wapo katika hali nzuri ya kimchezo na kwa pamoja wamepanga kuhakikisha wanapata ushindi utakaoitoa Tanzania kwenye nafasi ya 157 kwenye viwango vya ubora wa soka wa Dunia.

"Tuna morali wa hali ya juu,” alisema Mayanga ambaye aliteuliwa kuinoa timu hiyo mapema mwaka huu.

"Kikubwa ni ushindi ndio tunaoutegemea, tunafahamu wapinzani wetu wanataka ushindi, lakini tutatumia faida ya kucheza nyumbani kuipaisha Tanzania," alisema Mayanga.

Aidha, nahodha Samatta, alisema jana haitakuwa jambo jema kwa Stars kupoteza mchezo wa leo.

"Kama nilivyosema, tupo kwa ajili ya ushindi ingawa soka lina matokeo ya aina tatu..., tutapambana kwa nguvu zetu zote kupata ushindi," alisema Samatta.

Kwa upande wake, Kocha wa Botswana, Peter Buffler, aliweka wazi kuwa anatarajia mchezo mgumu hasa baada ya kugundua Stars kuwa na vijana wengi ikilinganishwa na miaka iliyopita.

SHARE THIS

0 comments:

Comment hapa